...

...

Wednesday, December 1, 2010

MAHOJIANO NA KHADIJA MWANAMBOKA JUU YA MIAKA MITATU YA TMH

Khadija Mwanamboka

Mwishoni mwa wiki iliyopita, kituo cha kulelea watoto yatima na wale wanaoishi katika mazingira magumu kilicho chini ya Tanzania Mitindo House(TMH), kilitimiza miaka mitatu(3) tangu kianzishwe.

Katika shamrashamra za kusheherekea miaka hiyo mitatu,BC ilipata nafasi ya kuongea na Bi.Khadija Mwanamboka,mbunifu maarufu wa mitindo nchini Tanzania ambaye pia ndio mwanzilishi wa kituo hicho ambacho kwa mujibu wa mahojiano niliyoyafanya naye miaka mitatu iliyopita,kuanzisha kituo kama hicho ilikuwa ni ndoto yake ya muda mrefu.

Ndani ya mahojiano haya,Khadija,anaongelea mambo mbalimbali hususani changamoto ambazo wamekabiliana nazo,mafanikio ambayo wameyapata tangu kuanzishwa kituo hicho na mipango yao ya baadaye.Fuatana nami katika mahojiano hayo;

BC: Bi.Khadija,kwanza kabisa nianze kwa kukupongeza wewe na watu wote wanaohusika na Tanzania Mitindo House(TMH) kwa kutimiza miaka mitatu. Je,ndani ya miaka mitatu iliyopita,mmekabiliana na changamoto zipi na unaweza kusema mpaka sasa mmepata mafanikio gani?

KM: Kwanza naomba nianze kwa kutoa shukrani,kwa niaba ya wenzangu wote tunaoshirikiana bega kwa bega katika kuendesha Tanzania Mitindo House.

Tukizungumzia mafanikio; Katika miaka mitatu iliyopita Tanzania Mitindo House imeweza kuboresha maisha ya watoto yatima ambao,kwa namna moja au nyingine, walishakata tamaa ya kuishi.Kutokana na kuwepo kwa kituo kama hiki, leo hii kila mmoja ana ndoto yake katika maisha.

Mafanikio mengine ambayo tumeyapata ni kwamba tumeweza kufikia lengo letu la kuwa na kiwanja cha kuchezea watoto yatima ili na wao wawe na uhuru wa kucheza na kufurahi kama watoto wengine walio na wazazi.

Pia tumeweza kutimiza lengo letu kuu la kusaidia jamii kwa kupitia mavazi au mitindo kwa kutangaza kazi zetu za ubunifu mikoani kama vile Dodoma ambapo tulifanya onyesho mwezi wa sita mwaka jana.Katika onyesho hilo,baadhi ya wabunge wetu walivaa mavazi yetu na kupita jukwaani kama wanamitindo. Pia tulifanikiwa kufanya onyesho la mavazi ambalo lilihudhuriwa na Rais wetu Jakaya kikwete kama mgeni rasmi kule Ngurdoto Arusha katika mkutano wa CPA. Vilevile kwa upande wa nje ya nchi, mwezi Octoba mwaka huu tulifanya maonyesho ya mavazi kule New Jersey na Washington DC nchini Marekani.

Changamoto kubwa inayotukabili ni ukosefu wa fedha ili kutimiza mipango mbalimbali tuliyonayo. Hapo ndipo tunapowaomba wahisani mbalimbali iwe ni mashirika ya umma au watu binafsi waendelee kujitokeza kutusaidia ili tutimize malengo mengi zaidi.

BC: Pamoja na juhudi za mashirika mbalimbali kama vile TMH katika kusaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu ikiwemo watoto wasio na wazazi,wanaoishi mitaani nk,bado matatizo hayo yapo na yanaendelea kukua.Je,una wito gani kwa washika dau mbalimbali,serikali nk katika kusaidia sio tu watoto ambao tayari wanaishi katika mazingira magumu bali pia kusaidia kukua kwa tatizo hili?

KM: Ni kweli kabisa unachosema. Tatizo hili bado lipo. Mimi nadhani kuna umuhimu wa kuendelea kutolewa kwa elimu kuhusu familia. Endapo wazazi wa mtoto wote wamefariki, basi ndugu wengine kama vile Baba Mdogo,Mjomba,Shangazi nk, wawe wepesi wa kujitolea kuchukua jukumu la kumlea mtoto aliyeondokewa na wazazi ambaye kimsingi ni ndugu/mtoto wao.Badala yake kinachotokea hivi sasa ni kwamba pindi tu mtoto anapoondokewa na wazazi,ndugu hukimbilia kuwapeleka katika vituo vya kulelea watoto yatima.Watoto wengi waliopo kwenye vituo,wana wajomba,mashangazi na ndugu wengine wenye uwezo wa kuwalea.Kuna haja ya familia kubadilika na kukubali jukumu la msingi la kuwalea watoto.
Baadhi ya watoto waliohudhuria sherehe za kutimiza miaka mitatu kwa TMH wakipata mlo.
BC: Kwa kifupi unaweza kuwaeleza wasomaji wetu aina za programu mlizonazo ndani ya TMH hususani zile zinazolenga katika kusaidia watoto wanaolelewa katika kituo cha TMH.Wanasoma au wanajifunza stadi zozote zile ambazo zitawasaidia katika siku za mbeleni maishani mwao?

KM: Watoto wote kumi tulionao kituoni wanaenda shule. Na wawili ambao ni mapacha Mungu akipenda wataanza sekondari mwakani.Hivi sasa wanasoma kiingereza. Mwalimu anakuja kila Jumamosi na Jumapili. Mwakani wataanza kusoma masomo ya computer pia mwalimu atakuwa anakwenda kituoni.

Vile vile kuna msichana (14) yeye ataanza kusomea kushona siku za Ijumaa jioni na mmoja mvulana (15) ataanza kusoma sanaa ya uchoraji.Wanapenda fani hizo nasi kama walezi tunapenda kuwaendeleza kimaisha.
Baadhi ya watoto wanaolelewa katika kituo cha TMH
BC: Miaka mitatu sasa imepita tangu TMH ianzishwe.Bila shaka kuna watu ambao ungependa kuwashukuru kwa michango yao ya hali na mali katika kuhakikisha kwamba TMH inaendelea kuwepo na inaendelea kusaidia jamii.Uwanja ni wako.

KM: Swali zuri sana.Kwanza napenda kumshukuru Danny Kiondo MEDIA,TMH DESIGNERS ESP HAJI MOHAMED na kisha wadhamini wote waliosaidia TMH na wanaoendelea kusaidia. Tunawashukuru Vodacom,Mr and Mrs Al Said,Benchmark Productions, RBP Oil company,Urban Pulse,i View Photography,Eventlites,Vayle Springs, Double Tree Hotel,wabunifu wote wa TMH, wanachama wote wa TMH na shukrani za dhati kwa vyombo vya habari vyote kwa ujumla na hasa bloggers; Familia yote ya kina Michuzi(The Great 3 Team-Muhidin,Ahmad na Othman) LadyJayDee, 8020 Fashions, MvutoKwanza, Dina Marios, Full Shangwe, Fashion Junkii,Vijimambo na bila kusahau BongoCelebrity(BC). Kwakweli wanatusaidia sana.

BC: Nini mipango ya TMH katika miaka labda mitatu au mitano ijayo?

KM: Mipango ni kufungua kiwanda kidogo cha kutenegneza nguo za wabunifu ndani ya TMH,kufanya maonyesho kila mwisho wa mwezi kuanzia mwakani na kuandaa sherehe ya Watoto Fun Day kila mwanzo wa mwezi mwakani.

BC: Kwa watu ambao hawakupata nafasi au fursa ya kusaidia TMH katika miaka mitatu iliyopita,unawaambia nini?Na kama wapo ambao watapenda kusaidia au kushiriki kwa njia moja au nyingine,wanatakiwa kufanya nini,kwa njia gani nk?

KM: Kwakweli kama nilivyosema mwanzo tunamipango mingi ila tunakwama fedha kwa hiyo tunaitaji msaada ili tuweze kufanikisha mipango hasa ili la Watoto Fun Day kuwafurahisha watoto yatima katika kituo chetu cha kuchezea kigamboni.

Kwanza naomba watu wapitie tovuti yetu www.mitindohouse.org na atakae mpenda kusaidia awasiliane na sisi kupitia info@mitindohouse.org

BC: Asante kwa muda wako Khadija,kila la kheri katika kazi zako.Tafadhali usichoke kuisaidia jamii.

KM: Asante Sana, Ubarikiwe




Kwa niaba ya bongocelebrity.


No comments:

Post a Comment