...

...

Sunday, December 6, 2009

Mtoto wa Osama bin Laden Akataliwa Kuoa Uingereza

Omar Bin Laden, mtoto wa kiongozi wa kundi la Al Qaeda, Osama Bin Laden
Mtoto wa kiume wa Osama bin Laden mwenye umri wa miaka 28 amenyimwa viza ya kuingia Uingereza kumuoa mchumba wake mwanamke wa Kiingereza mwenye umri wa miaka 54. Omar Bin Laden, mtoto wa kiongozi wa kundi la Al Qaeda, Osama Bin Laden anayetafutwa na Marekani kwa udi na uvumba, amenyimwa viza ya kuingia Uingereza kumuoa mchumba wake mwanamke mzaliwa wa Uingereza ambaye ana umri karibia mara mbili ya umri wake.

Omar Bin Laden alikata rufaa hukumu iliyotolewa mwaka jana ya kumnyima viza ya kuingia Uingereza kumuoa Jane Felix-Brown ambaye alisilimu na kupewa jina la Zaina.

Baba yake Omar, Osama Bin Laden ndiye anayetuhumiwa kuhusika na mashambulizi ya septemba 11 nchini Marekani ambayo yaliua mamia ya watu na mashambulizi katika balozi za Marekani nchini Kenya na Tanzania mwaka 1998 ambapo zaidi ya watu 200 walifariki.

Omar alifunga ndoa na Jane mwaka 2006 nchini Misri lakini ndoa yake ilikuwa haitambuliki kwa mujibu wa sheria za Uingereza kwakuwa Jane alikuwa ameolewa na mwanaume mwingine nchini Uingereza wakati huo na Omar alikuwa ana mke na mtoto nchini Saudia Arabia.

Kabla ya ndoa yao, Omar alikuwa ameoa na kuwaacha wanawake watano wakati Jane naye alikuwa ameolewa na kuachika mara nne.

Wakati wanafunga harusi yao nchini Misri, Jane alikuwa ndio yupo kwenye taratibu za kuachana na mume wake wa tano Andrew Yeomans.

Ingawa mahakama iliambiwa kuwa kwa mujibu wa sheria za kiislamu Jane alikuwa akihesabika ameachana na mumewe Bw. Yeomans lakini kwa sheria za Uingereza kuvunjika kwa ndoa yao kulitakiwa kuidhinishwa na mahakama. Hatimaye taratibu za mahakama kuivunja ndoa hiyo zilikamilika februari 2007.

Mwezi wa nne mwaka jana, Omar ambaye alidai hajawahi kumuona baba yake tangia mwaka 2000, alinyimwa viza ya kuingia Uingereza kwakuwa ndoa za kiislamu hazitambuliki kisheria nchini Uingereza.

Omar alikata rufaa na kuomba viza ya Uchumba ili amuoe mchumba wake kwa mujibu wa sheria za Uingereza ndani ya Uingereza lakini alinyimwa pia viza hiyo.

Omar aliambiwa kuwa baba yake jina lake kamili ni Osama Mohammed Awad bin Laden, ndiye anayetuhumiwa kuhusika na matukio mengi ya kigaidi duniani hivyo kuwepo kwake nchini Uingereza kutahatarisha amani.

Omar alikata rufaa tena akisema kuwa haki zake za kibinadamu zimevunjwa kwa kukataliwa kufunga ndoa na mchumba wake.

Hukumu iliyotolewa jana alhamisi ilizidi kumnyong'onyesha Omar na mpenzi wake kwani mahakama iliendelea kusisitiza kumnyima viza Omar ya kuingia Uingereza, ikisema kuwa mahakama haina uhakika kama kweli wapenzi hao wana nia ya kufunga ndoa ya kweli na kuishi pamoja.

Pia mahakama ilisema kuwa suala la baba yake Omar, Osama bin Laden kuwa gaidi anayetafutwa duniani limechangia yeye kunyimwa viza.

Akizungumzia hukumu hiyo Jane alisema "Nina wajukuu lakini niko tayari nikae nao mbali ilimradi niwe karibu na Omar".

Omar ni mtoto wa nne kati ya watoto 11 wa Osama bin Laden aliozaa na mke wake wa kwanza. Osama bin Laden inasemekana ana jumla ya watoto 19.
Kwa hisani ya jamiiforums
.........................................................................................

No comments:

Post a Comment