...

...

Sunday, November 8, 2009

HAYA HUU NDIO ULIMWENGU WA MAPENZI



Jambo hilo ni kawaida kabisa na huwasumbua wengi sana katika kufanya maamuzi sahihi. Wengi hushindwa na kubaki wanababaika na sehemu ya kusimamia!
Wanaokumbana na tatizo hili zaidi ni wanawake ambao wanakosa njia sahihi za kueleza hisia zao na badala yake ama kukubali kuendelea kupata usumbufu na kero ama kuporomosha matusi kwa mwanaume huyo wakiamini ni dawa kumbe wanakosea sana!

Ijulikane wazi kwamba, kila mmoja ana haki ya kupenda, lakini si kila anapopenda mtu lazima na yeye apendwe! Unaweza ukapenda sehemu usiyopendwa au ukapendwa na usiyempenda! Kikubwa kinachohitajika hapa ni jinsi gani unavyofikisha hisia zako kwa mhusika.

Hapo ndipo wengi wanapokosea. Je, wewe ni mwanamke ambaye unasumbuliwa na mwanaume ambaye siyo chaguo lako? Hata kama siyo, unajua cha kufanya siku utakapotokewa na hali hiyo?
Ondoa shaka, hapa nimekuandalia mambo muhimu sana ambayo kama ukiyafuatilia na baadaye kuyatumia kwa makini, basi jambo hili halitakusumbua kabisa! twende pamoja...

KUBALI WITO...
Hili linawashinda wengi, lakini kumbuka Waswahili walisema; ‘Kubali wito, kataa neno.’ Inawezekana kabisa umeshajaribu kumwangalia jamaa na ukagundua kuwa anakuhitaji kimapenzi na wewe mwenyewe kutoka moyoni mwako unaamini kuwa hayupo katika moyo wako, sawa!

Lakini kukubali kwako kumsikiliza hakutoi tafsiri kuwa tayari umeshamkubalia. Kubali wito, nenda ila jitahidi kukwepa sehemu zenye vificho au ambayo utakuwa na wasiwasi nayo. Utakapokubali utamfanya mwanaume huyu aone hujamdharau na unamheshimu.

MWACHE AELEZE HISIA ZAKE...
Kuna wengine wanaweza wakafaulu vizuri hatua ya kwanza ya kukubali wito, ila akifika tu ataanza kumwuliza; “Sema haraka ulikuwa unasemaje?” au “Nina haraka bwana zungumza haraka ulichoniitia,” hayo na maneno mengine yanayofanana na hayo hayana maana, mwache azungumze, usimkatishe kauli. Msikililize mwanzo mpaka mwisho.

Onyesha kujali mazungumzo yake na kuwa makini kwa kila anachozungumza japokuwa tayari moyoni unatambua kuwa haupo tayari kuwa naye kimapenzi. Hakikisha anafahamu kuwa mawazo yako yapo pale, hii itamfanya jamaa kuwa huru kwako na kukueleza hisia zake kwa uwazi zaidi.

HESHIMU HISIA ZAKE
Hii ni hatua muhimu kuliko zilizotangulia. Ni wazi kuwa baada ya kumpa nafasi azungumze, alikutamkia kuwa anakutaka! Ukweli uliopo katika moyo wako ni kwamba humuhitaji kwa namna yoyote. Mshukuru kwa kukupenda, onyesha kumthamini, onyesha imani juu yake.

Onyesha masikitiko kutokana na jibu utakalompa kwa sababu ni wazi kuwa hatalipenda! Hii itamfanya mwanaume huyo ajione wa thamani ila kwa bahati mbaya alichelewa! Onyesha kuthamini alichozungumza na jitahidi kuonyesha hisia za kuwa ni kijana mtanashati lakini kwa bahati mbaya sasa una mwenyewe (hata kama huna).

MWAMBIE UKWELI
Mpaka amefikia hatua ya kutoa dukuduku lake moyoni na kukutamkia bayana kuwa anakuhitaji, ni wazi kuwa mwanaume huyu anakupenda. Sasa kama ndivyo na imetokea bahati mbaya hana sifa unazozihitaji, usimjibu vibaya, tumia akili yako ya kuzaliwa kuweza kufikisha hisia zilizopo katikati ya moyo wako lakini asijisikie vibaya.

Unaweza kumwambia; “Asante sana kwa kunipenda, hata mimi nakupenda pia, lakini kwa bahati mbaya umewahiwa, nina mchumba ambaye nampenda na yeye ananipenda na siyo vizuri kumsaliti,” hakika huu ndiyo msumari wa mwisho!

Kama mwanaume huyo ni muelewa hawezi kukusumbua tena. Kama alikuwa ni mwanaume mwenye mapenzi ya kweli kwako na siyo wa kukuchezea atathamini maneno yako kutokana na ukweli halisi uliompa hasa ukizingatia kuwa kama yeye ndiye angekuwa anasalitiwa asingejisikia vizuri.

MTAKE RADHI
Lazima utakuwa umempotezea muda wake mwingi kukutana na wewe na kuzungumza pamoja. Isitoshe inawezekana mazungumzo yenu mlikuwa mkizungumzia katika Hoteli, Mgahawa au mahali pengine ambapo jamaa alitumia gharama zake hivyo kuhisi kuwa amepotezea fedha zake bila mafanikio.

Kubwa zaidi utakuwa umemwacha na majeraha makubwa katika moyo wake hasa kama na yeye alikuwa akikupenda kwa dhati. Baada ya kumweleza hali halisi, mtake radhi kwa kumpotezea muda wake, pia mwambie asikuchukie na mbaki kama kaka na dada.

Hapo utakuwa umemwacha mwanaume huyu katika hali nzuri ya kutojisikia vibaya au kushushwa thamani yake tofauti na kutumia maneno makali au matusi.

No comments:

Post a Comment